Ethiopia yawatesa wafungwa wa kisiasa

Image caption Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Mamlaka nchini Ethiopia wanadaiwa kuwatesa na kuwatendea vibaya mahabusu wa kisiasa kwa lengo la kuwalazimisha kukiri makosa Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Human Right Watch limesema.

Shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani limesema wafungwa walishikiliwa katika mahabusu kuu katikati ya mji mkuu wa Adis Ababa wamesema wamekuwa wakichapwa na kupigwa mateke wakati wa mahojiano.

Shirika hilo linaishutumu Ethiopia kwa kutumia sheria ya kupinga Ugaidi kuwakandamiza wapinzani.

Hata hivyo serikali ya Ethiopia imetupilia mbali madai ya ripoti hiyo na kusema kuwa imeegemea upande mmoja na kukosa ushahidi wa kutosha, Shirika la Habari la AP limesema.

Ripoti ya Shirika hilo la Haki za binadamu limesema polisi wanaofanya upepelezi katika gereza la Maekelawi wamekuwa wakitumia njia haramu za kuwahoji watuhumiwa, kuwaweka wafungwa walioshikiliwa katika mazingira mabaya na kuwazua kuwasiliana na wanasheria.

Mmoja kati ya mahabusu amenukuliwa akisema " amekuwa akishikiliwa katika eneo la mateso kwa masaa kadhaa, kuning'inizwa kwenye ukuta wakati akipigwa bakora", taarifa hiyo imesema.