Shehena ya meno ya tembo yanaswa Uganda

Maafisa nchini Uganda wamekamata shehena meno ya tembo yenye uzito wa tani mbili, ambacho ni kiwango kikubwa kukamatwa kwa miaka mingi iliyopita.

Chama cha Wanyama Pori nchini Uganda kimesema meno yapatayo 832 yenye thamani ya dola milioni 6.7 yamekamatwa.

Wataalamu wanasema baadhi ya meno hayo yanaaminika yametokana na tembo waliouawa na majangili nje ya nchi ya Uganda.

Kuna mahitaji ya meno ya tembo kutoka barani Afrika kwenda nchi Asia kwa ajili ya kutengeneza mapambo.

Meno hayo ya tembo yalikuwa yakielekea kwenda kusafirishwa katika bandari ya Mombasa nchini Kenya.

Baadhi ya meno hayo yalikuwa yamekatwa vipande vipande na kufunikwa na chupa za plastiki kwenye makreti na kubandikwa maandishi kuonyesha kwamba ni bidhaa zinazokwenda kuchakatwa (recycling).

Chama hicho cha Wanyama pori kimemwambia mwandishi wa habari wa BBC Catherine Byaruhanga kuwa Uganda imeanza kutumiwa na majangili kama njia ya kupitisha bidhaa za wanyamapori kutoka nchi za Sudan Kusini na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.