Wapiganaji wasakwa na kuuwawa Tunisia

Majeneza ya askari wa Tunisia waliouwawa Alkhamisi

Wizara ya ulinzi ya Tunisia imesema kwamba watu kama 9 wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wameuwawa na tani mbili za mabomu zimekamatwa, katika msako uliofanywa na jeshi karibu na pahala ambapo askari polisi wawili waliuwawa Alkhamisi.

Msako huo ulifanywa katika eneo la Mlima Taouye, kilomita 70 magharibi ya Tunis, na karibu zaidi na mji mkuu kushinda katika mapambano yaliyofanywa kabla na wapiganaji wa Kiislamu.

Ijumaa Waziri Mkuu, Ali Larayedh, na Rais Moncef Marzouki walizuwiliwa kuhudhuria mazishi ya polisi hao wawili na askari wa usalama waliokuwa wakiandamana.

Viongozi wa Tunisia wa chama cha Kiislamu na vyama vya upinzani wataanza mjadala wa taifa Jumatano, ili kumaliza msukosuko wa kisiasa ulioko nchini.