Ethiopia kulinda haki za binadamu

Image caption Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Serikali ya Ethiopia inasema kuwa itazindua mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa, siku kadhaa baada ya ripoti mpya kutuhumu serikali hiyo kwa ukatili dhidi ya wafungwa wa kisiasa.

Waziri wa sheria Berhanu Tsegaye anasema kuwa mkakati huo ulibuniwa kujaza pengo zilizoko katika kuhakikisha kuwa serikali inaheshimu haki za binadamu.

Nchi hiyo imekuwa ikituhumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia sheria za kupambana na ugaidi kukandamiza watu.

Kwa miaka mingi, serikali ya Ethiopia imetuhumiwa kwa kukiuka haki za binadamu ikiwemo kuwazuilia watu na kuwatesa kikatili.

Lakini serikali inasema kuwa mpango wake wa kwanza kuhusu haki za binadamu utayozinduliwa Ijumaa, itasaidia sana katika kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanywa awali kuhusiana na haki za binadamu.

Tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu, imekuwa ikituhumiwa kwa kupuuza hali ya maelfu ya wanaharakati wa upinzani na waandishi wa habari wanaozuiliwa nchini humo.

Ripoti iliyotolewa na shirika la Human Rights Watch, imesema kuwa kambi rasmi ya kuwazuilia watu, mjini Addis Ababa,alielezea kuchapwa na kupigwa mateke wakati akihojiwa.

Serikali hata hivyo imepuuza ripoti hiyo na kusema ina mapendeleo na kuwa haina ushahidi wa kutosha.

Miongoni mwa wale waliohojiwa, Martin Schibbye, mwandishi wa habari mwenye uraia wa Sweden anasema alishtakiwa kwa kuwa nchini humo kinyume ne sheria na kuunga mkono kundi la waasi.

Maandamano yalifanyika kwenye barabara za mji nchini Ethiopia mwezi Juni kutaka waandishi na wanaharakati kuachiliwa.

Haya yalikuwa maandamano ya kwanza makubwa kufanyika mjini Addis Ababa tangu mwaka 2005 wakati mamia ya waandamanaji waliuawa kwenye maandamano hayo.