Wanamageuzi wajitoa serikalini Sudan

Ghasia katika maandamano mjini Khartoum ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta

Wanamageuzi maarufu katika chama tawala cha Sudan wametangaza kuwa wanatoka chamani kuunda chama kipya, ishara kuwa mzozo umezidi ndani ya serikali.

Wanaharakati hao wamelalamika juu ya ukandamizaji wa maandamano ya hivi karibuni ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo.

Piya wamekishutumu chama cha Kiislamu cha National Congress kwamba kinakwenda kinyume na misingi yake.

Kati ya waliotoka ndani ya chama ni aliyekuwa mshauri wa Rais Omar al-Bashir.

Mwandishi wa BBC mjini Khartoum anasema serikali ya Sudan inapata shida kumudu uchumi unaozidi kuzorota, hasa kwa sababu ya kukosa pato kutokana na mafuta baada ya Sudan Kusini kujitenga mwaka wa 2011.