Viongozi wa EAC kukutana Kigali Rwanda

Image caption Jumuiya ya Afrika Mashariki imekumbwa na msukosuko bada ya TZ kupuuza mikutano inayofanya ikisema inakiuka utaratibu wa jumuiya

Wakuu wa nchi za Kenya,Uganda na Rwanda baadaye leo wanatarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajiwa kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka Mombasa Kenya -- Uganda hadi Rwanda.

Kuundwa kwa Kituo hicho pia kunatazamiwa kurahisisha shughuli nzima za uchukuzi katika maeneo hayo ya Afrika Mashariki.

Taifa la Sudan Kusini pia linataraji kuidhinishwa kama mshirika katika kikao cha wakuu wa mataifa hayo.

Mkutano huu unalenga kuimarisha maendeleo ya kikanda kupitia kwa miundo msingi bora , uchumi na biashara.

Shughuli hii inakuja baada ya mkutano uliofanyika mjini Kampala Uganda, mnamo mwezi Juni na mwengine uliofanyika mjini Mombasa mnamo mwezi Agosti ambako viongozi walipendekeza kupanuliwa kwa bandari ya Mombasa ili kuwezesha uharaka wa bidhaa kupitishiwa bandarini humo katika kuhudumia kanda nzima.

Tanzania awali ilipuuza mikutano ya Kenya ,Uganda na Rwanda ikisema kuwa ni kinyume na utaratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kando na hayo mkutano mwengine wa marais wa nchi nane utafanyika Kesho ambapo watakutana kwenye kongamano la siku nne mjini Kigali ambalo linatarajiwa kuweka kipaombele kwa uimarishwaji wa huduma za internet katika mataifa hayo.

Mkutano huo unaofanyika miaka sita baada ya Kigali kuwa mwenyeji wa kongamano la Connect Africa, mwenyeji wake atakuwa Rais Paul Kagame na Dr Hamadoun I. Toure, katibu mkuu wa muungano wa kimataifa wa mawasiliano ya kiteknolojia (ITU)

Marais hao ni pamoja na Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Salva Kiir wa Sudan Kusini Ali Bongo Ondimba wa Gabon, Thomas Boni Yayi wa Benin na Rais Blaise Compaore wa Burkina Faso .

Mkutano huo unaanza rasmi Kesho.

Nchi zengine 15 za Afrika zitashiriki kwenye mkutano huo ambao kwa mujibu wa waandalizi, zaidi ya wajumbe 1,500 watahudhuria.