Mwakilishi wa UN azuru Syria

Image caption Mwakilishi wa UN kwenye mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi

Mpatanishi wa mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi, anafanya ziara jijini Damascus ikiwa ni mara ya kwanza baada ya takriban mwaka mmoja.

Ziara yake inamadhumuni ya kutafuta kuungwa mkono katika mkutano wa maswala ya amani unaotarajiwa kufanyika mjini Geneva mwezi Novemba.

Chanzo cha habari cha Umoja wa mataifa kimeiambia BBC kuwa Brahimi atakutana na Rais wa Syria, Bashar Al Assad katika ziara yake ya siku tatu nchini humo.

Mkutano wa Geneva utahusisha mazungumzo ya kwanza ambayo yatahusisha upinzani wa Syria.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-Moon, amesema Syria ina mpango wa kuteketeza vifaa vya kutengeneza silaha zake za kemikali mwishoni mwa mwezi huu.

Katika hatua nyingine wachunguzi wa kimataifa walioko nchini humo wamesema kuwa sababu za kiusalama zimezuia jopo lao kutembelea maeneo mawili ambayo Serikali ya Syria iliwaruhusu kuingia.

Shirika la kuzuia matumizi ya silaha za kemikali (OPCW) limesema kuwa uchunguzi wao umekamilika katika maeneo 21 kati ya 23.