Waiba dola milioni 54 Libya

Image caption Mji wa Sirte umekuwa ukikumbwa na visa vya wizi tangu mapinduzi ya kijeshi kung'oa mamlakani hayati Gadaffi

Shirika la habari la serikali nchini Libya limeripoti kuwa watu waliokuwa wamejihami wameiba dola milioni 54 kutoka kwa gari lililokuwa linapeleka pesa hizo kwenye benki kuu ya Libya.

Watu hao kumi walisimamisha gari hilo lilipokuwa linaingia mjini Sirte kutoka katika uwanja wa ndege. Pesa hizo zilikuwa zimetoka umbali wa kilomita 500 kutoka uwanja wa ndege mjini Tripoli.

‘‘Wizi huo ni pigo kubwa sana kwa watu wa Libya,’’ alisema Abdel-Fattah Mohammed, kiongozi wa baraza la Sirte.

Libya imekuwa ikikumbwa na visa vya wizi na uhalifu mwingine tangu kutokea harati za mapinduzi mwaka 2011.

Serikali imekuwa ikikumbwa na wakati mgumu kudhibiti hali ya usalama hasa kutokana na makundi ya wahalifu na wapiganaji wa kiisilamu yanayosakama nchi hiyo.

Ripoti zilisema kuwa gari moja pekee la ulinzi ndilo lilikuwa limeandamana na gari hilo wakati wizi huo ulipofanyika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Lana, walinzi walishindwa kukabiliana na wezi hao kumi .

Takriban dinar milioni 53 sarafu za Libya ziliibwa pamoja na dola milioni 12 za kimarekani ikiwemo sarafu za Euro.

Benki mbili mjini Sirte pia zilikumbwa na wizi mwezi Julai.

Wezi hao walifanikiwa kuiba dinar nusu milioni .

Mji wa Sirte ulikuwa ngome ya hayati kanali Muammar Gaddafi wakati wa mzozo wa kisiasa uliomwondoa mamlakani.