Shambulizi la kujitoa mhanga Tunisia

Polisi nchini Tunisia wanasema kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga, amejilipua nje ya hoteli moja ya kitalii ya Sousse.

Mshambuliaji huyo aliuawa lakini wafanyakazi wa hoteli hiyo walinusurika. Hakuna mtu aliyejeruhiwa kwenye shambulizi hilo.

Mji wa Sousse ni eneo muhimu sana la kitalii, Kusini mwa mji mkuu Tunis na liko umbali wa kilomita 140 kutoka mji mkuu katika pwani ya Miditerrania.

Mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo aliambia BBC kuwa shambulizi lililtokea karibu na hoteli.

Mshambuliaji aliyekuwa mwanamume, alikuwa amevalia ukanda wenye mabomu na yeye peke yake ndiye aliyefariki.

Wakati huohuo, polisi wamemzuilia mshambuliaji aliyejaribu kujilipua katika kaburi la aliyekuwa rais wa nchi hiyo Habib Bourguiba,mjini Monastir.

Mji huo uko umbali wa kilomita 20 katika pwani ya Sousse.

Bwana Bourguiba aliongoza Tunisia baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa ingawa aliondolewa mamlakani mwaka 1987 na kufariki miaka 13 iliyopita.