Wakamatwa kwa kashfa ya ARV's A. Kusini

Image caption Dawa za ARV hutolewa bila malipo katika vituo vya afya vya serikali Afrika Kusini

Maafisa wawili wa afya nchini Afrika Kusini wamekamatwa baada ya kuwauzia wagonjwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.

Kwa mujibu wa polisi, dawa hizo hazipaswi kuuzwa bali hutolewa bila malipo kwa waathiriwa wa virusi vya HIV katika hospitali za umma.

Polisi wa kitengo maalum, walifanya uchunguzi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wagonjwa.

Wanaume hao watashitakiwa kwa makosa ya wizi na kupatikana na dawa zinazopaswa kutolewa bure kwa wagonjwa.

"Wagonjwa walilazimika kutoka hospitalini bila dawa katika hospiali ya Esselen baada ya kuambiwa kuwa hakuna dawa za ARV. Kisha baadaye walishauriwa na maafisa wawili wa afya waliowaambia kuwa wanaweza kuwauzia dawa hizo,’’ shirika la habari la Sapa lilimnukuu msemaji wa kitengo hicho maalum cha polisi, kapteni Paul Ramaloko.

Bwana Ramaloko alisema kuwa washukiwa walikuwa wanauza dawa hizo kwa dola sita kwa boxi moja ndogo na waliwambia wagonjwa kuwa dawa hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwa wakati wa dharura.

Maafisa hao watafikishwa mahakamani Ijumaa. Uchunguzi ulianza mnamo mwezi Mei na kukamilishwa Septemba.

Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg amesema kuwa ukubwa wa operesheni ya polisi dhidi ya madai hayo haujulikani wala ukubwa wa kashfa hiyo.

Wanaume hao, walikamatwa Jumatano, baada ya kuwauzia dawa maafisa wa ujasusi.

"Wale waliokamatwa lazima wakabiliwe na sheria kwa vitendo vyao," alisema Simon Zwane, msemaji wa idara ya afya katika mkoa wa Gauteng,’’ liliripoti gazeti la Sapa.

Afrika Kusini ni moja ya nchi zenye idadi, kubwa ya waathiriwa wa virusi vya HIV duniani na maafisa wa afya nchini humo wanasema kuwa ina mpango mkubwa zaidi wa kutoa dawa za ARV duniani.