Japan na Urusi kushirikiana zaidi

Image caption Mawaziri wa Urusi wakishikana mikono na wenzao wa Japan

Japan na Urusi zimekubaliana kukuza ushirikiano kati ya majeshi yao.

Baada ya mazungumzo mjini Tokyo, waziri wa mambo ya nje wa Japan, Fumio Kishida, amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Asia Mashariki, ambako nchi mbili hizo zina ushawishi mkubwa.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema ushirikiano wao hautaathiri ushirikiano uliopo kati ya Japan na Marekani.

Habari zinasema Urusi imekuwa ikiongeza biashara na mataifa ya Asia na imekuwa ikitafuta uhusiano wa karibu zaidi na Japan, ikiwa ni kudhibiti kukua kwa ushawishi wa China katika eneo hilo.

Ijumaa Japan na Urusi zilikubaliana kuendelea kulitafutia ufumbuzi suala la mgogoro wa mpaka, ambalo limezuia mataifa hayo kutia saini mkataba wa amani, ambao unamaliza rasmi uhasama wao wa vita vikuu vya pili vya dunia.