Kenya yaahidi hatua dhidi ya wabakaji

Maandamano yaliyofanywa Kenya juma hili kupinga adhabu waliyopewa wabakaji

Wakuu wa Kenya wameahidi kuchukua hatua za haraka baada ya watu wa sehemu mbalimbali za dunia kuonesha hasira juu ya ubakaji wa kikatili aliofanyiwa msichana wa miaka 16.

Inadaiwa kuwa wanaume sita walimnajisi msichana huyo ambaye alipoteza fahamu, na kisha kumtupa kwenye lindi.

Watatu kati ya waliokamatwa walipewa adhabu ya kukata majani tu nje ya kituo cha polisi.

Jaji mkuu wa Kenya, Willy Mutunga, alisema ameipeleka kesi hiyo mbele ya shirika linalosimamia polisi na mahakama, National Council for the Administration of Justice, NCAJ.

Watu zaidi ya milioni wametia saini malalamiko kwenye mtandao kudai haki katika kisa hicho.