Mapigano mapya yazuka DRC

Image caption Maelfu ya wananchi wamelazimika kutoroka makwao kutokana na mapigano makali yanayoendelea mpakani mwa DRC na Uganda

Mapigano makali yamezuka kati ya majeshi ya serikali ya Congo na waasi wa M23 katika mpaka wa mashariki na taifa la Uganda.

Mapigano makali yameripotiwa kutokea wakati majeshi hayo ya serikali yanapojaribu kuchukua udhibiti wa maeneo yaliosalia mikononi mwa waasi wa M23.

Mwandishi wa BBC Issac Mumena aliyeko katika eneo hilo la mpaka wa Uganda na DRC anasema kuwa mapigano hayo yamesababisha maelfu ya wakimbizi kuvuka na kuingia nchini Uganda kutafuta usalama na matibabu kwa wale waliojeruhiwa.

Waasi wa M23 mnamo siku ya Jumapili walitoa wito kwa wapiganaji wao kusitisha vita ili kuruhusu mazungumzo ya amani kufanyika kati ya viongozi wa kundi hilo na waasi hao.

Hata hivyo, kwa mujibu mwa mwandishi wa BBC hakuna dalili ya kufanyika mazungumzo ya amani.

Anasema kuwa hali ni tete sana katika eneo la mpakani.

Inaarifiwa kuwa waasi hao wanaonekana kujibu vikali mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi wa serikali na hali ni mbaya kuliko siku za awali, na taarifa zinasema kuwa wanajeshi wanakaribia kushinda vita vyao dhidi ya waasi hao.

Mapigano ya hivi sasa yanakuja baada ya wanajeshi wa serikali kudhibiti baadhi ya miji iliyokuwa imetekwa na waasi hao baada ya kuwafurusha.