Waathriwa hawataki kesi ya Uhuru kuahirishwa

Image caption Baadhi ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi waliopoteza makao yao kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi 2007

Mwakilishi maalum wa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya , katika mahakama ya kimataifa ya ICC, ameandika ujumbe wa dharura kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa akiwataka wanachama wa baraza hilo kukataa ombi la kuakhirisha kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Rasimu ya azimio iliyoandikwa na Rwanda imetolewa kwa baraza hilo kabla ya mkutano kuhusu ombi la Kenya kuanza Rasmi.

Zaidi ya wakenya elfu moja waliuawa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwak 2007-2008.

Rais Kenyatta na naibu wake pamoja na mwanahabari Joshua Sang wamekanusha madai dhidi yao ya kuchochea ghasia hizo na kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.

Kwenye ujumbe wake ambao BBC iliweza kuuona, mwakilishi wa waathiriwa na mashahidi Fergal Gaynor anaonya kuwa uikiwa kesi hizo zitacheleweshwa , kutakuwa na tisho kubwa kwa masilahi ya waathiriwa.

Anawasilisha ombi hilo bada ya stakabadhi iliyoandikwa na Rwanda kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kuungwa mkono na nchi za Muungano wa Afrika, unaotaka kesi hiyo kuakhirishwa kwa sababu ya kustawisha amani na usalama Kenya pamoja na katika maeneo ya upembe wa Afrika.

Azimio hilo linazungumzia maswala ya kigaidi na hata kugusia shambulizi la hivi karibuni lililotokea katika jumba la Westgate mjini Nairobi kama ushahidi wa tisho wanalozungumzia la usalama wa nchi.

Lakini wakili wa waathiriwa anatetea kuwa kucheleweshwa kwa kesi hizo , kutakwenda kinyume na majukumu ya UN ambayo ni pamoja na kuhakikisha kuna uthabiti, pamoja na kuhakikisha kuwa viongozi wanotumia nguvu ili kuepuka kuchukua hatua za kisheria kwa uhalifu waliotenda.

Chini ya kifungu cha 16 cha mkataba wa Roma njia pekee ya Kenya kupata afueni ni baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuahirisha kesi dhidi ya viongozi hao chini ya sheria za kimataifa.

Ili kesi hiyo kuahirishwa, wanachama wa baraza la usalama la UN watahitajika kupigia kura hoja hio.

Rais Kenyatta anatarajiwa kwenda Hague Februari mwaka ujao, wakati kesi dhidi yake itakapoanza.

Hata hivyo wakili anasema kuwa ikiwa kesi hiyo itaakhirishwa kwa mwaka mmoja, wengi wa waathiriwa ambao waliambukizwa virusi vya HIV, kutokana a ubakaji huenda wakafariki kabla ya kutoa ushahidi wao.