Rupiah Banda: Sikuhusika na ufisadi

Image caption Rupiah Banda aliongoza Zambia kwa miaka mitatu

Rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda, amekana mashitaka katika kesi inayomhusisha na ufisadi wakati wa kampeini za uchaguzi wa mwaka 2011.

Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 76, anatuhumiwa kupokea lori 10 kutoka kwa tawi moja la kampuni ya ujenzi ya kichina na kukosa kutangaza kuwa alipokea lori hizo.

Baada ya miaka mitatu mamlakani ,Banda alishindwa na rais wa sasa Michael Sata katika uchaguzi wa mwaka 2011.

Hii ni kesi ya pili ya ufisadi inayomkumba Banda tangu kuondolewa kinga dhidi ya kushitakiwa mnamo mwezi Machi.

"ninaelewa mashitaka na ninayakanusha ,'' alisema Banda alipofikishwa mbele ya hakimu na kusomewa mashtaka dhidi yake.

Inadaiwa kuwa rais huyo wa zamani, alisajili lori hizo alizopokea kutoka kwa kampuni ya kichina ya Anhui ,kwa majina ya jamaa zake pamoja na mfuasi wake mmoja na kisha kuyatumia wakati wa kampeni zake mwaka 2011.

Serikali ya Rais Sata imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi dhidi ya waliokuwa viongozi katika serikali ya Banda.

Lakini wakosoaji wa Rais Sata wanasema kuwa anatumia mbinu hii kuwakandamiza wakosoaji wake.

Mnamo mwezi Machi, Banda pia alikana mashitaka ya ufisadi dhidi yake kuhusu mkataba aliotia saini na kampuni ya mafuta ya Nigeria ambayo viongozi wa mashtaka wanaamini ulinuiwa kufaidi familia ya Banda.