Fulana yaleta kero kwa kijana Angola

Image caption Dos Santos ametawala Angola tangu mwaka wa 1975

Kijana mmoja aliyekamatwa miezi miwili iliyopita kwa kushonesha fulana zilizokuwa na maandishi ya kusema kuwa Rais Jose Eduardo dos Santos ni Dikteta, ameanza kususia chakula.

Wakili wa kijana huyo kwa jina Manuel Chivonde Nito Alves alisema kuwa ameamua kususia chakula kwa sababu ya ukatili anaofanyiwa akiwa kizuizini.

Alves alikuwa ametengeza fulana hizo kwa sababu ya maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kupinga utawala wa Dos Santos, ambayo polisi waliyasambaratisha mwezi Septemba.

Ameshitakiwa kwa kosa la kumtusi Rais. Rais Dos Santos, ameitawala nchini hiyo yenye utajiri wa mafuta tangu mwaka 1975.

Katika miaka miwili iliyopita,kumekuwa na maandamano kadhaa ya kupinga serikali.

Licha ya uchumi wa nchi hio kukuwa, raia wengi wangali wanaishi katika umasikini mkubwa