Meya aliyevuta Cocain akataa kujiuzulu

Image caption Meya Rob anasema anajiandaa kwa uchaguzi wa meya mwaka ujao

Meya wa mji mkubwa nchini Canada,Toronto, Rob Ford, ameomba msamaha kwa wakaazi wake baada ya kukiri kwamba kwa wakati mmoja alivuta cocaine.

Ford aliwaambia waandishi habari kwamba kukiri kwa kile alichokitaja kuwa ni kosa lake ni jambo lililo gumu na lenye aibu ambalo amewahi kufanya.

Lakini amesema hatojiuzulu na kwamba ataendelea na kampeini za kugombea nafasi hiyo mwaka ujao .

Awali, Meya huyo aliwaambia waandishi kwamba alivuta dawa hiyo ya kulevya katika maskani ya kulewa takriban mwaka mmoja uliopita.

Kanda ya video inayomuonyesha meya huyo akivuta Cocaine ilizuka mnamo mwezi Mei lakini awali Ford alikana tuhuma hizo.

Wiki iliyopita mkuu wa polisi mjini Toronto alisema aliipata nakala ya kanda hiyo ya video.

Hata hivyo aliomba radhi na kusema kuwa anaipenda sana kazi yake na mji wa Toronto. ''Najua jambo nililolifanya lilikuwa baya sana na itanibidi niweze kurejesha imani yenu kwangu.''

Alisema kuwa aliificha tabia yake kutoka kwa familia na wafanyakazi wenzake.

''Ni mimi wa kulaumu kwa haya yote,'' bwana Ford aliwaambia waandishi wa habari. ''Na ninaahidi kuwa jambo kama hili halitawahi kutokea tena.''