Je wataka hisa za twitter?

Image caption Wadadisi wanasema mtandao wa Twitter unahitaji kujiimarisha kama mitandao mingine ili upate faida

Mtandao wa kijamii wa Twitter umetangaza kuuza hisa zake kwa dola 26 kila hisa , kabla ya kuanza kuziuza rasmi katika soko la hisa la New York baadaye leo.

Bei hiyo iko juu ya kiwango kilichotabiriwa cha dola 23 kwa kila hisa ambacho kilitangazwa mnamo siku ya Jumatatu.

Thamani ya mtandao huo inasemekana kuwa dola bilioni 18.

Twitter ina watumiaji milioni 230 tangu huduma hiyo kuanza kutolewa miaka minane iliyopita, ingawa bado haijapata faida yoyote.

Mtandao huo ulipata hasara kubwa mwaka huu na kulingana na kura ya maoni, zaidi ya thuluthi moja ya watu waliojisajiLI na mtandao huo hawautumii kamwe.

Hata hivyo, inaonekana watu wengi walitaka sana kupata hisa za kampuni hiyo na hivyo ikaweza kuiweka kwenye soko la hisa la New York.

Wadadisi wanasema kuwa waekezaji wana matumaini ya mtandao huo kukuwa kwa kasi katika siku zijazo.

"waekezaji wanaona mitandao ya kijamii na simu za mkononi kuwa mahala pa kuchovya asali, na ndio maana tamko tu la kuuza hisa za kampuni hiyo linawachangamsha sana watu.''

Hata hivyo, wadadisi wanahisi kuwa mtandao huo unapaswa kujiimarisha zaidi kutokana na matumaini waliyonayo wakezekaji.

Kampuni hiyo, imefanikiwa kupata mauzo zaidi na inatarajiwa kuongeza mauzo hayo kutoka kwa wafanyabiashara nje ya Marekani.

Baadhi wanasema kuwa bei ya hisa hizo itapanda baada ya kuwekwa katika soko la hisa.

"kama tu mitandao ya Google, Amazon na Facebook ilizovyojiimarisha kuwa vifaa muhimu vya kutumia kwenye internet, Twitter nayo inaelekea katika njia hio hio.''