Msomali akamatwa kuhusu ajali ya Lampedusa

Image caption Watu 366 walifariki katika ajali ya Lampedusa

Polisi nchini Italia, wamemkamata raia moja wa kisomali mwenye umri wa miaka 24 aliyehusishwa na ajali ya Lampedusa ambapo zaidi ya waafrika miatatu walifariki baada ya boti waliyokuwa wanafiria kuzama katika kisiwa cha Lampedusa.

Mwanamume huyo, anayeaminika kuwa mwanachama wa genge moja la wahalifu, anatuhumiwa kuwa mmoja wa watu wanaoendesha biashara haramu ya binadamu.

Alikamatwa kisiwani humo.

Mtu anayedaiwa kuwa mmiliki wa boti hiyo, raia wa Tunisia kwa jina Khaled Bensalam, alikamatwa na sasa anazuiliwa mjini Sicily.

Wengi wa waathiriwa wa ajali hiyo iliyotokea Oktoba tarehe tatu walikuwa raia wa Eritrea na wasomali.

Boti hiyo iliyokuwa imesongamana watu, ilianza kuteketea na kisha kuzama karibu na ufuo wa kisiwa hicho kidogo kilichoko Kaskazini mwa Afrika.

Watu 155 walinusurika.

Vyombo vya habari nchini Italia vimesema kuwa mwanamume mmoja raia wa Italia alikamatwa na polisi mjini Roma. Kwa sasa inaarifiwa anahojiwa mjini Sicily.

Mshukiwa alikuwa anajidai kuwa mhamiaji aliyekuwa anatoroka vurugu na umaskini nchini mwake , kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Italia.

Lakini manusura wa ajali hiyo walimtaja kuwa mmoja wa wale waliopanga safari hiyo.