Idadi ya vifo Ufilipino yapungua

Image caption Waathirika wa kimbunga Ufilipino

Serikali ya Ufilipino imesema zaidi ya watu elfu moja mia nane wamethibitika kufa kufuatia kimbunga Haiyan.

Rais Benigno Aquino amesema anafikiri idadi ya awali iliyotajwa kuwa watu elfu kumi wameuawa katika kimbunga Haiyan ilikuwa kubwa mno, akisema idadi halisi huenda ikawa watu elfu mbili na mia tano.

Lakini kauli ya Rais Aquino inapingana na maelezo ya maafisa kadha ambao wansema idadi iliyotolewa mwanzoni ya watu elfu kumi kufa kutokana na kimbunga Haiyan ni sahihi.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na maafisa wa usimamizi wa majanga, zinaonyesha kuwa zaidi ya nyumba elfu themanini na watu wapatao laki sita hawana makaazi.

Wakati huo huo, watu wanane wameuawa nchini Ufilipino wakati watu walionusurika katika kimbunga Haiyan walipojaribu kuvamia ghala la kuhifadhia mchele ili kujipatia chakula.

Watu hao wamekufa wakati ukuta wa jengo ulipoporomoka katika mji wa Tacloban ulioharibiwa vibaya kutokana na kimbunga Haiyan.

Mbunge mmoja kutoka eneo hilo, Martin Romualdez, ameonya kuwa watu wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji na dawa.

Pia amesema kuvunjwa kwa sheria na kanuni nyingine za usalama kunakwamisha usambazaji wa misaada na kwamba hali ya dharura inatakiwa kuchukuliwa na serikali kuu.

Bwana Romualdez amesema mji wa Tacloban umeharibiwa vibaya, mithili ya kupigwa na bomu la nyuklia na kwamba utalazimika kujengwa upya kabisa.