Naibu wa mkuu wa usalama atekwa Libya

Wanamgambo wa Libya

Naibu wa mkuu wa usalama wa Libya, Moustapha Nouh, ametekwa nyara kutoka uwanja wa ndege wa Tripoli alipokuwa akirudi nchini.

Kamanda mmoja piya alitekwa lakini aliweza kukimbia na alieleza kuwa walitekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha.

Afisa huyo ametekwa wakati kunafanywa mgomo katika mji mkuu kuwahimiza wapiganaji waondoke katika mji huo.

Mgomo umefanywa baada ya zaidi ya watu 40 kufa na mamia kujeruhiwa kwenye mapambano ya siku mbili baina ya wanamgambo na waandamanaji, ambao wamewaomba wanamgambo waondoke mjini.

Waziri Mkuu, Ali Zeidan, alitekwa nyara kwa muda mfupi mwezi uliopita.