Washambuliaji wa Westgate walivyopenya Kenya

Wanamgambo wanne wa kundi la Al Shabaab waliohusika na shambulizi la kigaidi dhidi ya jumba la Westgate nchini Kenya , waliingia nchini Kenya kupitia mpakani kutoka Somalia.

Afisaa mmoja mkuu kutoka mojawapo ya nchi za Magharibi ameambia BBC kuwa wanamgambo hao waliingia nchini Kenya kupitia eneo ambalo hutumiwa na watu wengi kuingia Kenya na kisha kukita kambi katika mtaa wa Eastleigh, mjini Nairobi.

Mtaa huo una wahamiaji wengi wa Kisomali baadhi waliokimbia vita kutoka Somalia.

Washambuliaji wanasemekana waliishi Somalia kwa muda ambako walipata mafunzo yao.

Watu 67 waliuawa kwenye shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la Al Shabaab dhidi ya jumba la maduka la Westgate katika mtaa wa Westlands mnamo mwezi Septemba.

Al Shabaab lilikiri kufanya shambulizi hilo kwa lengo la kulipiza kisasi dhidi ya serikali ya Kenya kwa kutuma majeshi yake nchini Somalia kupambana dhidi ya kundi hilo.

Hadi kufikia sasa raia wanne wa kigeni wamefikishwa mahakamani baada ya kuhusishwa na shambulizi hilo. Wanadaiwa na polisi kuwapa makao washambuliaji hao mjini Eastleigh.

Washukiwa hao, Mohammed Ahmed Abdi, Liban Abdullah, Adan Adan na Hussein Hassan wamekanusha madai ya kuwapa hifadhi magaidi na kuwasaidia kufanikisha mipango yao.

Afisaa huyo hata hivyo amesisitiza kuwa ni watu wanne pekee walioshambulia jengo hilo kama ambavyo serikali ya Kenya imekuwa ikisisitiza.

Wawili kati ya wale waliofanya shambulio hilo, wamejulikana kutokana na nyaraka za mahakani wakisemekana kuwa Hassan Dhuhulow, anayeaminika kuwa raia msomali mzaliwa wa Norway na Mohammed Abdinur Said.

Washambuliaji hao walikuwa na kile maafisa wa usalama wanasema ni msaada mkubwa ndani ya Kenya.

Lakini hakuna ushahidi kuonyesha kuwa mshukiwa mkuu wa ugaidi, Samantha Lewthwaite, mzaliwa wa Uingereza ambaye ni mjane wa mshambuluaji aliyeshambulia kituo cha treni mjini London Uingereza mwaka 2005, alihusika na shambjlizi hilo.

Taarifa hizi zinaweza kusaidia majasusi kujua uraia halisi wa washukiwa wa shambulizi hilo na uhusiano wao na kundi la kigaidi la Al Shabaab.