Askari wa Misri washambuliwa Sinai

Image caption El-Arish

Askari kumi wa Misri wameripotiwa kuuawa na wengi kujeruhiwa kutokana na kulipuliwa na bomu karibu na mji wa el-Arish kaskazini mwa Sinai nchini Misri.

Gazeti la Al-Masri al-Youm limesema msafara wa mabasi yakiwa yamebeba askari wa miguu ulipigwa na bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara wakati msafara huo ukielekea katika eneo la Kharouba.

Idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo huenda ikaongezeka, imesema taarifa ya vyombo vya usalama.

Mashambulio dhidi ya askari wa usalama katika eneo la Sinai, kaskazini mwa Misri yameongezeka tangu Rais Mohammed Morsi ang'olewe madarakani mwezi Julai mwaka huu.

Hali ya usalama katika eneo hilo imezidi kuzorota katika miaka ya karibuni, ikichochewa na kuangushwa kwa Rais Hosni Mubarak. Kuondolewa kwake madarakani mwezi Februari 2011 kulisababisha eneo la kaskazini mwa Sinai kulengwa na vikundi vya wapiganaji, vikundi vingine vikihusishwa na wapiganaji wa ukanda wa Gaza, huko Palestina.

Mwezi Septemba, majeshi ya usalama yalianzisha mashambulio dhidi ya wapiganaji wa Kiislam huko Sinai, lakini majeshi hayo yalikabiliwa na mashambulio makali ya mabomu.

Shambulio la Jumatano, ambalo lilitokea saa 01:45 asubuhi kwa saa za huko katika barabara inayotoka Rafah kwenda el-Arish, linafikiriwa kuwa shambulio baya kabisa kufanyika dhidi ya jeshi la Misri tangu Bwana Morsi aondolewe madarakani.

Tovuti ya gazeti la al-Ahram imeripoti kuwa askari 26 wamejeruhiwa katika mlipuko huo.

Shambulio hili limeripotiwa kulenga askari wa kikosi cha jeshi la Misri, ambao wametumwa katika eneo la Sinai na wamehusika katika operesheni ya kuharibu njia za chini ya ardhi zilizopo kati ya mpaka wa Misri na ukanda wa Gaza.

Askari walioshambuliwa walikuwa wakirejea Cairo kuanza likizo zao. Baadhi ya askari waliojeruhiwa vibaya, walichukuliwa kwa ndege kupelekwa katika hospitali, mjini Cairo.