CAR imesisitiza inazungumza na Kony

Image caption Marekani inasema kuwa madai ya Kony ni kiini macho tu

Serikali ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati imesisitiza kuwa imefanya mazungumzo na kiongozi wa waasi, Joseph Kony baada ya Marekani kuelezea shauku kuwa Kony amehusika katika mazungumzo na serikali ya CAR bali ni waasi wake pekee.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Msemaji wa serikali ya CAR Guy-Simplice Kodegue hata hivyo alisema kuwa Rais Michel Djotodia amefanya mazungumzo na Kony mmoja wa wahalifu wa kivita ambaye amekuwa mbioni mwa miaka mingi.

Inaarifiwa mazungumzo yanahusu hali ya watoto walioingizwa katika kundi la wapiganaji la Kony LRA kwa lengo la kuwa wapiganaji,

Kony amekua kisakwa na mahakama ya kimataifa ya ICC, tangu mwaka 2005 kwa madai ya ubakaji, utumwa wa kingono, mauaji na kuwatumia watoto kama wanajeshi.

Mnamo siku ya Alhamisi, maafisa wakuu nchini Marekani walielezea shaka kuhusu taarifa za kiongozi wa waasi wa LRA nchini Uganda kufanya mazungumzo na serikali ya Jamuhuri ya Afrika ya kati kuhusu kutaka kujisalimisha.

Rais wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati ambako Kony amejificha na waasi wake amesema kua Kony, anayesakwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na mahakama ya jinai ICC, amefanya mazungumzo na serikali yake.

Afisa kutoka katika wizara ya mambo ya ndani nchini Marekani, ameambia BBC kuwa waasi kadhaa walishauriana na serikali ya CAR wala sio Kony mwenyewe.

Marekani iliahidi kutoa zawadi ya dola milioni 3.3 kwa mtu yeyote mwenye taarifa ambayo ingepelekea kukamatwa kwa Kony.

Kony alianzisha kundi la waasi la LRA, kaskazini mwa Uganda, zaidi ya miaka 20 iliyopita, na waasi wake wanasifika kwa kuwateka nyara watoto na kuwaingiza katika kundi lao la waasi kama wapiganaji pamoja na kuwa watumwa wa ngono.

Maafisa hao walielezea kuwa Kony amewahi kutumia mbinu zote kama hizi kupumzika, kujikusanya upya na waasi wake na hata kujihami upya na kisha kuanza kuteka nyara, kuua na kusababisha watu kutoroka makwao.

Waasi wa LRA walilazimika kutoroka Uganda mwaka 2005 na tangu hapo wamekuwa wakifanya vurugu katika CAR, Sudan Kusini na katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Nusura Joseph Kony atie saini mkataba wa Amani mwaka 2008 lakini akasisitiza kuwa mahakama ya ICC mwanzo itupilie mbali kibali cha kumkamata , ingawa mahakama hiyo ilikataa kufanya hivyo.