Joseph Kony ataka kujisalimisha?

Majeshi ya Marekani yanayoshauri wanajeshi wa Uganda  katika msako dhidi ya Kony
Maelezo ya picha,

Majeshi ya Marekani yanayoshauri wanajeshi wa Uganda katika msako dhidi ya Kony

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya kati inasema inajadiliana na kiongozi aliyetoroka wa waasi kutoka Uganda Joseph Kony.

Msemaji wa serikali ameiambia BBC kwamba Joseph Kony alikuwa katika Jamhuri ya Afrika ya kati, lakini alitaka kuhakikishiwa usalama wake kabla hajajisalimisha.

Marekani imekuwa ikivisaidia vikosi vya Uganda kumsaka Kony.

Kony, ni kiongozi wa kundi la waasi la LRA, na anatakikana na mahakama ya kimataifa ya jinai kwa madai ya uhalifu wa kivita.

Marekani ilikuwa imeahidi kumtuza dola milioni 3.3 yeyote mwenye taarifa itakayopelekea kukamatwa kwa Kony

Hii ni mara ya kwanza kwa miaka mingi, kwa taarifa kuhusu aliko Kony kutolewa.

Pia mnamo siku ya Jumatano, mjumbe maalum wa muungano wa Afrika kuhusu LRA, Francisco Madeira, aliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa, kuwa aliona ripoti kuwa Kony anaugua ugonjwa mbaya sana usiojulikana.

Mnamo mwezi Aprili, jeshi la Uganda lilisitisha msako dhidi ya Kony katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, likisema kuwa linabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa serikali waasi walipochukua mamlaka baada ya mapinduzi.

Joseph Kony pamoja na wapiganaji wake walio kati ya 200-500, wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Uganda kwa zaidi ya miaka 20.