Rais Goodluck Jonathan hospitalini London

Image caption Goodluck anakumbwa na migawanyiko chamani wapinzani wake waking'ang'ania mamlaka

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan anaendelea kupokea matibabu mjini London lakini wasaidizi wake wamesema kuwa hali yake sio mbaya sana.

Rais Goodluck alikwenda mjini London kwa mkutano , ingawa hakuweza kuhudhuria mkutano wenyewe.

"tungependa kuwahakikishia kuwa Rais Jonathan hayuko katika hali mbaya,'' alisema msaidizi wake Reuben Abati

Alisema kuwa matibabu aliyokuwa anapokea rais huyo mwenye umri wa miaka 56 ni ya kuzuia tu hali yake kuwa mbaya.

Rais Jonathan amekuwa Rais tangu mwaka 2010, baada ya mtangulizi wake hayati Umar Yar Adua kufariki akiwa mamlakani.

Wakati huo alikuwa makamu wake wa Rais na hivyo kuchukua hatamu za uongozi.

Rais alilazimika kuchelewesha siku yake ya kusoma bajeti, ya kila mwaka bungeni baada ya toafuti kati ya serikali na bunge kuibuka.

Bwana Jonathan pia anakumbwa na migawanyiko mikubwa chamani huku wapinzani wake wakilumbania madaraka kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Pia anakabiliwa na wakati mgumu kupambana dhidi ya harakati za kundi la wapiganaji wa Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria.