Picha za Nyumba ya Zuma magazetini SA

Image caption Jopo la wahariri limetaja onyo hilo la serikali kama la kipuuzi sana

Magazeti nchini Afrika Kusini yamepchapisha picha za nyumba ya Rais Jacob Zuma, na kupuuza onyo la serikali kuwa jambo hilo linakiuka sheria za usalama.

Nyumba hiyo ya Zuma iliyo katika mtaa wa Nkandla imesababisha mjadala mkali baada ya serikali kusema kuwa ilitumia dola milioni 12 pesa za umma kuifanyia ukarabati.

Mawaziri wa serikali walisema nmao siku ya Alhamisi kuwa yeyote atayechapisha picha ya nyumba hiyo atakamatwa.

Jopo la wahariri nchini humo lilitaja onyo hilo kama la kipuuzi sana.

Moja ya magazeti yaliyocgapisha picha hiyo, Jarida la Times leo limekuwa na kichwa '' Basi tukamateni '' juu ya picha ya nyumba ya kifahari ya Zuma.

Nalo gazeti la The Star lina picha ya nyumba ya Zuma ikiwa na msalaba mwekundu huku maandiko yakisema,'' Usitizame, kile ambacho mawaziri wa serikali hawataki ukione.''

Waziri wa usalama Siyabonga Cwele alisema mnamo siku ya Alhamisi kua , hakuna mtu anayeruhusiwa kupiga picha nyumba ya Rais ikiwemo vyombo vya habari na kusema kuwa huo ni uvunjaji wa sheria za usalama.

''Hilo halifanyiki popote duniani. Hatujaona picha za ikulu ya White house ambayo ina ulinzi mkali. Hilo halifanyiki katika nchi yoyote yenye kutii demokrasia,'' alisema waziri huyo

Onyo hilo limezua hasira miongoni mwa wananchi, wengi wakielezea kughadhabishwa na hata kuziweka picha hizo kwenye mtandao wa Twitter.