Polisi wapambana na wavamizi Kenya

Polisi nchini Kenya wanaendesha operesheni dhidi ya wavamizi walioteka kijiji kimoja Kaskazini Magharibi mwa nchi.

Walisema kuwa wavamizi hao wamejihami kiasi cha haja na waliweza kukabiliana nao ingawa hali bado ni tete.

Kijiji hicho kiko katika eneo ambalo hukumbwa na makabiliano ya kila mara kati ya watu wa jamii ya Turkana na Pokot wakizozania mali asili.

Inaarifiwa washambuliaji waliwazuia watu 900 wengi wakiwa watoto na wanawake katika vijiji vinne, katika jimbo la Turkana Kusini kwa karibu wiki moja.

Polisi wa kupambana na ghasia na polisi wa kawaida wamekwenda katika eneo hilo wakiwa wamebeba chakula kufuatia ripoti kuwa mamia ya wanakijiji pamoja na kikosi cha polisi, hawana chakula na maji na hali imekuwa hivyo kwa karibia wiki moja.

Mmoja wa viongozi wa eneo hilo, alisema kuwa wavamizi hao waliwazuia watu wa jamii ya Turkana bada ya mzozo kuhusu umiliki wa ardhi inayokaliwa na jamii hiyo kudaiwa kuwa mali ya jamii ya Pokot.

Naibu kamishna wa jimbo hilo anasema kuwa mzozo huu huenda uliibuka baada ya kutolewa ramani mpya kuhusu mpaka kati ya eneo la Pokot Magharibi na jimbo la Turkana Kusini.

Polisi hata hivyo walikana ikiwa kuna watu waliotekwa nyara na washambuliaji hao katika kijiji cha Lorogon.

Polisi waliokwenda katika eneo hilo kudbihiti hali walisema walikutana na vijana karibu miambili kutoka jamii ya Pokot waliokuwa wamejihami na kuweka vizuizini barabarani.

Kulikuwa na makabiliano makali kati ya polisi na washambuliaji hao wikendi yoyote.

Duru zinasema kuwa mazungumzo kati ya jamii hizi mbili yalitarajiwa kuanza siku ya Jumapili lakini hakuna taarifa kuhusu ikiwa yalianza au la.

Wanasiasa katika jimbo hilo wanasema hali ya kibinadamu heunda ikawa mbaya zaidi hasa baada ya kijiji cha Lorogon kuzingirwa kwa siku nne sasa.