Wakosoa sheria ya kupinga maandamano Misri

Image caption Maandamano yamekuwa yakitokea Misri kila kukicha

Makundi ya kutetea haki za binadam nchini Misri yamelaani vikali sheria mpya ya kuzuia maandamano ya umma iliyotiwa saini na Rais wa mpito Adly Mansour.

Sheria hiyo inayopiga marufuku maandamano yanayoandaliwa bila ya kuwapa polisi taarifa, inalenga haswa wafuasi wa kundi lililopigwa marufuku la Muslim Brotherhood na ambalo lina wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani, Mohammed Morsi.

Maandamano ya umma yamesababisha kupinduliwa kwa serikali za rais 2 wa misri katika kipindi cha miaka 3, na haya yanajiri wakati maandamano zaidi yakiendelea katika miji tofauti ya Misri siku ya Jumapili huku wafuasi wa Bwana Morsi wakikusanyika katika mji wa Cairo na miji mingine.

Wafuasi hao walikua wanaadhimisha siku 100 tangu vikao vikitaka kurejeshwa kwa Mohammed Morsi.

Mapambano hayo yalisababisha vifo vya mamia ya watu.

Kisa kingine cha maandamano jijini Cairo kilisababisha mapigano baina ya polisi na waandamanaji waompinga Morsi siku ya Ijumaa.

Morsi ambaye ana mizizi katika siasa za kiislamu anakumbwa na mashtaka pamoja na wanachama wengine wa kundi la undugu wa kiislamu kwa madai ya uchochezi na vifo. Makundi ya kutetea haki za kibinadam nchini Misri yameipinga rasimu ya sheria hiyo kabla ya kutungwa na Rais wa mpito Mansour.

Katika taarifa kutoka kwa mashirika 19 nchini misri, ''rasimu ya sheria hiyo inataka kuhalifisha mikusanyiko yote ya amani ikiwemo maandamano na mikutano ya umma na inaipa serikali mamlaka ya kutawanya mikutano ya amani kwa kutumia fujo.''

Akizungumza na shirika la habari la AFP, waziri mkuu wa misri, Hazem Beblawi alisema kuwa sheria hii mpya imeundwa ili kulinda haki za waandamanaji na hivyo kuwataka kuwapa polisi taarifa lakini si kuomba ruhusa.

Duru za serikali zilinukuliwa zikisema kuwa kipindi cha kutolewa kwa taarifa kuhusu sheria hiyo kimepunguzwa kutoka siku 7 hadi 3.

Chaguzi za ubunge na urais zinatarajiwa kufanyika mwaka ujao lakini makundi ya kutetetea haki za kibinadam yameshtumu uongozi unaoungwa mkono na jeshi kwa tabia zinazodhulumu demokrasia.

Maelfu ya wanachama wa kundi la undugu wa kiislamu wamezuiliwa tangu kuondolewa kwa rais Morsi lakini serikali yasema kuwa hii ni njia ya kupambana na ugaidi.