Waandamanaji Thailand wadhibiti wizara

Image caption Waandamanaji nchini Thailand

Waandamanaji katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok wameendelea kulenga wizara za serikali, wakidhibiti baadhi ya majengo na mengine kuyazingira, wakipinga utawala wa waziri mkuu, Yingluck Shinawatra.

Hati ya kukamatwa imetolewa dhidi ya kiongozi mmoja wa waandamanaji akihusishwa na hatua ya waandamanaji hao kukalia majengo ya wizara za serikali.Wakati huo huo bunge la Thailand linajadili hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Bi Yingluck.

Waandamanaji wanasema wanalenga kukwamisha shughuli za serikali kwa lengo la kumlazimisha waziri mkuu kujiuzulu. Wanasema Bi Yingluck ni kibaraka wa kaka yake, Thaksin Shinawatra ambaye alikuwa waziri mkuu wa zamani wa Thailand aliondolewa madarakani kwa njia ya maandamano.