Miraa haizidishi ugaidi

Mbunge Florence Kajuju
Image caption Mbunge Kajuju anasisitiza miraa hainufaishi ugaidi

Akiwaongoza wabunge wenzake katika kulishawishi bunge la Uingereza kutopitisha sheria za kupiga marufuku miraa kutoka Kenya kuingia nchini Uingereza, mbunge Florence Kajuju, kutoka jimbo la Meru nchini Kenya, ameielezea BBC akiwa London kwamba uchunguzi wao unaonyesha mapato ya biashara ya miraa kamwe hayana uhusiano na ugaidi.

Ameelezea kwamba utafiti wao umegundua kwamba kuna kampuni mbili tu ambazo huingiza miraa nchini Uingereza, na hakuna ushahidi wowote kuonyesha mapato yao hutumiwa katika kuendeleza ugaidi.

Kuhusiana na madai ya athari za afya, anasema wamezungumza na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na ambao wamesema miraa haina hatari zozote za kiafya.

Anasema miraa haiwezi kufikiriwa kama mihadarati.

"Ile kitu imetufurahisha zaidi ni kwamba ripoti iliyofikishwa katika bunge la Uingereza kutoka kwa kamati inayotoa ushauri kuhusiana na utumizi usiofaa wa dawa ilisema ya kwamba miraa sio dawa ya kulevya na kwa hiyo haikuielezea serikali ya Uingereza ipige marufuku miraa", alielezea.

Mbunge Kajuju anasema kwa kiasi fulani, ujumbe wao umeanza kuwashawishi baadhi ya wabunge wa Uingereza na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa zao la miraa, na kwamba haina athari zozote za kiafya.

Lakini anaelezea kazi yao sio rahisi, kwani "huyu mama ambaye ni waziri wa masuala ya nyumbani wa Uingereza ameendeleza, na amefikisha muswada bungeni akiomba sheria ipitishwe ya kupiga marufuku miraaa na ndio sababu tuliona ni afadhali tuje na tuzungumze na wabunge wenzetu tuwaelezee na kuleta ripoti tuliyoileta kutoka Kenya kutoka kwa wanasayansi wetu wa Kenya kuwaonyesha kwamba miraa haina shida yoyote".

Zao la miraa linategemewa sana kiuchumi na wakulima wengi katika maeneo ya Meru na Embu nchini Kenya.