UN: Kutumia ndege zisizo na rubani DRC

Image caption Marekani imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani kupambana na makundi ya wanamgambo Somalia, Pakistana na Afghanistan

Majeshi ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameanza kutumia ndege zisizo na rubani kuchunguza harakati za waasi katika mipaka na Rwanda na Uganda.

Hii ni mara ya kwanza kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa kutumia ndege za aina hiyo.

Ndege mbili za kwanza zilirushwa kutoka mji wa mashariki wa Goma ambao mwaka jana ulikaliwa kwa muda mfupi na waaasi wa kundi la M23.

Ndege mbili za kwanza zinaundwa na shirika la Italia la Selex ES.

Jeshi la Umoja wa mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ndio kubwa kupita yote duniani na lilichangia kwa kiasi kikubwa mwezi uliopita ushindi dhidi ya waasi wa kundi la M23;lakini bado kuna makundi mengine kadhaa ya wanamgambo nchini humo.

Kikosi kipya kilichoimarishwa nguvu cha Umoja wa Mataifa kilitumia ndege za helikopta kulisaidia jeshi la Congo dhidi ya waasi hao wa M23.

Eneo tajiri la madini la mashariki mwa Congo limekumbwa na vita kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita lakini kushindwa kwa M23 kumeleta matumaini fulani ya kupatikana utulivu zaidi kwa eneo hilo.

Mwandishi wa BBC, mashariki mwa Congo Maud Jullien amesema kwa muda mrefu kumekuwa na tuhuma kwamba vikundi mbalimbali vyenye silaha katika jimbo la Kivu Kaskazini wakipata msaada kutoka nchi jirani.

Rwanda na Uganda mara kwa mara zimekanusha tuhuma za kuwasaidia waasi wa M23, kikundi ambacho hivi karibuni kilipigwa na majeshi ya Congo yakisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa vinavyolinda amani nchini Congo.

Askari wapatao 22,000 wapo nchini Congo, kikiwa ni kikosi kikubwa zaidi cha Umoja wa Mataifa katika shughuli za kulinda amani duniani.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kulinda amani Herve Ladsous ameiambia BBC kuwa ndege hizo zisizo na rubani, zitatumika kama njia mojawapo ya kufuatilia harakati za makundi yenye silaha na mienendo ya raia katika eneo la mashariki mwa Congo.

"Tunatakiwa kuwa na picha halisi ya kile kinachotokea," amesema.

Amesema kama watafanikiwa nchini DR Congo, ndege hizo zinaweza pia kutumika katika maeneo mengine ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.