Viongozi duniani wamlilia Nelson Mandela

Image caption Nelson Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Alhamisi usiku alitangaza kifo cha rais wa kwanza mweusi nchini humo, Nelson Mandela, ambaye amefariki dunia tarehe 5 Desemba 2013 akiwa na umri wa miaka 95.

Rais Zuma anasema, "Mpendwa wetu Nelson Rolihlahla Mandela, mwasisi wa taifa letu la kidemokrasia, ameaga dunia. Ameondoka kwa amani akiwa na familia yake saa mbili na dakika 50 usiku kwa saa za Afrika Kusini, tarehe 5 Desemba 2013. Kwa sasa anapumzika. Kwa sasa ana amani.

"Taifa letu limempoteza mtoto wake mkuu wa kiume. Watu wetu wamempoteza baba. Licha ya kwamba tulifahamu kuwa siku kama hii ingemtokea, hakuna kinachopunguza upendo wetu kwake na hasara kubwa tuliyopata. Jitihada zake kutafuta uhuru zimemjengea heshima kubwa duniani.

"Unyenyekevu wake, upendo wake na utu wake, vimesababisha watu kumpenda. Mawazo yetu na sala zetu tunazielekeza kwa familia ya Mandela. Kwao tuna deni kubwa la kuwashukuru. Walijitolea kwa kiasi kikubwa na kuvumilia mengi ili watu wetu wawe huru. Amesema Zuma.

"Mawazo yetu yapo pamoja na mkewe Gra├ža Machel, mke wake wa zamani Winnie Madikizela-Mandela, pamoja na watoto wake , wajukuu wake na familia nzima. Mawazo yetu yapo pamoja na rafiki zake, marafiki katika mapambano na washirika wake walioshirikiana na Madiba katika mapambano ya ukombozi.

"Mawazo yetu yapo pamoja na wananchi wa Afrika Kusini ambao leo wanaomboleza kifo cha mtu,ambaye zaidi ya wengine amekuja kuleta hisia ya taifa moja. Mawazo yetu yapo pamoja na watu duniani kote ambao wamemkubatia Madiba kama mtu wao, na ambaye aliona matatizo yao ni yake.

Taifa letu limempoteza mtoto wao muhimu sana.

"Kile kilichomfanya Nelson Mandela kuwa kiongozi mkuu ni kile hakika kilichomfanya awe na utu. Tumeona ndani yake kile tunachokitafuta ndani mwetu. Na ndani yake tumeona mengi tunayohitaji.

Image caption Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

"Ndugu zangu Afrika Kusini, Nelson Mandela alituleta pamoja na pamoja tunamuaga.

"Mpendwa wetu Madiba atapewa mazishi ya kitaifa. Nimeshaagiza kuwa bendera zote nchini Afrika Kusini zitapepea nusu mlingoti kuanzia tarehe 6 Desemba na kubakia hivyo hadi baada ya mazishi yake. Wakati tukikusanyika kutoa heshima zetu za mwisho, hebu twende kwa utu na heshima ambayo Madiba alijijengea. Hebu tufikirie matarajio yake na matarajio ya familia yake.

"tukiwa tumekusanyika, popote tulipo duniani, tukumbuke mambo ambayo Madiba alipigania. Hebu tuthibitishe dira ya jamii, ambayo ndani yake hakuna anayenyonywa, kukandamizwa au kunyanyaswa na mtu yeyote.

"Hebu tujibiidishe bila kupoteza nguvu kujenga Afrika Kusini yenye umoja, isiyo na ubaguzi wa rangi, isiyo na ubaguzi wa kijinsia, Afrika Kusini ya kidemokrasia na ustawi. Hebu tueleze kwa namna yetu wenyewe, shukrani kubwa tuliyonayo kwa mtu ambaye ametumia muda mwingi kuwatumikia watu wa nchi hii na kwa minajili ya utu.

"Huu kwa kweli ni wakati wa masikitiko makubwa".

Lakini lazima pia uwe wakati wa maana kwa yale tuliyodhamiria.

Image caption Wananchi Afrika Kusini waomboleza kifo cha Mandela

"Dhamira ya kuishi kama alivyoishi Madiba, kupambana kama Madiba alivyopambana na bila kupumzika hadi tutakapofikia kile alicholenga katika kujenga Afrika Kusini yenye umoja, Afrika yenye amani na ustawi na dunia bora zaidi. Daima tutampenda Madiba! Roho yako ipumzike kwa amani. Mungu Ibariki Afrika.

Naye waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ametuma rambirambi kwa Rais Jacob Zuma kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Amesema: "mwangaza mkuu umetoweka duniani. Nelson Mandela alikuwa shujaa wa wakati wetu."

Bendera katika ofisi za waziri mkuu zinapeperushwa nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kumheshimu.

Bwana Cameron anasema"Kukutana naye lilikuwa moja ya mambo ya heshima kubwa katika maisha yangu.

Image caption David Cameron, waziri mkuu wa Uingereza

"Moyo wangu umeelekezwa kwa familia yake na kwa watu wote nchini Afrika Kusini na kwingineko duniani.

Kwa upande wake Rais Obama wa Marekani ameungana na wabunge na marais wa zamani kuomboleza kifo cha Nelson Mandela, akimtaja kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi zaidi, jasiri na mtu mwema kuwahi kuishi.

"Amepata zaidi ya kile kilichotarajiwa kutoka kwa mtu yeyote. Leo amekwenda nyumbani," Obama akiwa amegubikwa na majonzi alisema katika taarifa aliyoitoa Ikulu ya Marekani.

"Si wetu tena. Ni wa vizazi vyote."Asema Obama.

Rais Obama ametaka bendera zote nchini humo zipeperushwe nusu mlingoti hadi Jumatatu jioni, ili kutoa heshima kwa kiongozi huyo mpinga siasa za ubaguzi wa rangi.

Naye Rais wa zamani wa Marekani, George H.W. Bush alielezea mshangao na kuona mtu wa aina yake Nelson Mandela kwa kuwa na uwezo wa kusamehe watu waliomfunga miaka 27 jela bila makosa, akitoa fundisho kwa sisi sote kuweza kusamehe hata maadui zetu."

Naye rais mwingine wa zamani wa Marekani, Bill Clinton amesema marehemu Mandela atakumbukwa kama kinara wa utu wa binadamu na uhuru kwa amani na maridhiano."

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-amempongeza Nelson Mandela kama mtu mnyenyekevu na mafano wa kuigwa na binadamu.".

Image caption Rais Barack Obama wa Marekani

"Nelson Mandela alikuwa mtu wa aina yake duniani, mtu mwenye utu na aliyefikia mafanikio ya juu, mwamba wa haki na mnyenyekevu.

"nimesikitishwa sana na taarifa za kifo chake. Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, ningependa kutuma rambirambi zangu kwa watu wa Afrika Kusini na hususan familia ya Nelson Mandela na wapendwa wake.

Katika ujumbe wake Rais wa China Xi Jinping ameelezea kusikitishwa kwake na kifo cha Nelson Mandela, ambaye amefariki dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 95, huku akitaakia subira familia ya Nelson Mandela. Bwana Xi amesema wananchi wa China, daima watakumbuka mchango usio wa kawaida wa Bwana Mandela katika kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika Kusini kwa maendeleo ya watu wa nchi mbili hizo.

Tanzania imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2013, kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Rais Jakaya Kikwete pia ameagiza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

"Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu". Amesema Kikwete.

Bwana Kikwete amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Image caption Rais Xi Jinping wa China

"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wananchi wa Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake". Rais ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".

Kutoka Kenya, Rais Uhuru Kenyatta anasema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha 'Shujaa' Nelson Rolihlahla Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini na kinara wa Afrika.

Amesema kwa niaba ya serikali na watu wa Jamhuri ya Kenya ameelezea masikitiko makubwa kwa familia na marafiki wa Nelson Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, huku akiwataka wananchi wa Afrika Kusini kuwa na moyo wa uvumilivu katika wakati huu mgumu.

Rais wa zamani wa nchi hiyo Mwai Kibaki amesema wakati dunia inapata habari za kusikitisha za kifo cha Nelson Mandela, Afrika itakuwa inasherehekea kuwa na kiongozi wake shupavu katika karne ya 20 na 21. Anasema Mandela alishinda ubaguzi wa rangi na kufafanua maana halisi ya uhuru na kuchochea viwango vipya vya utu wa kiafrika na undugu. Alikuwa mfano bora wa matumaini na dunia iliyo na usawa.

waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Raila Odinga anasema Nelson Mandela anasema ni mmoja wa binadamu wachache ambao wanaangalia mbele na unakutana nao mmoja katika karne moja au kizazi kimoja na pale tu tunapokuwa tumebahatika kuwapa watu wa aina hiyo. Alikuwa mstahamilivu, shupavu, mnyenyekevu, mwenye kujaa matumaini na mvumilivu. Tuna bahati kwamba tumeishi na kumshuhudia akipata umaarufu na kuwa mfano angali hai.