Gwiji wa Rumba Tabu Ley azikwa Kinshasa

Image caption Tabu lei alijulikana kwa utunzi wake na uimbaji wa muziki wa Rumba

mazishi ya Gwiji wa Rumba nchini DRC, Tabu Ley Rochereau yalifanyika Jumatatu mjini Kinshasa.

Mwili wake ukiwa ndani ya jeneza la rangi nyeupe lililotandwa bendera ya Jamhuri ya Congo, ulilazwa kwenye majengo ya Bunge ambako watu zaidi ya elfu kumi walifika kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Pascal Sinamoyi Tabu Ley.

Viongozi wa serikali ya DRC walihudhuria mazishi hayo huku waakilishi kutoka nchi jirani ya Congo Brazaville pia wakihudhuria mazishi hayo.

Tabu Ley alifariki mwezi Novemba akiwa na umri wa miaka 76 akipokea matibabu nchini Ubelgiji.

Aidha gwiji huyo alikiri rasmi kwamba ana watoto 49.

Lakini mwandishi wa BBC katika mazishi hayo Lubunga Byaombe, alisema kuwa zaidi ya watu 80 walijitokeza na kusema kuwa baba yao ni mwanamuziki huyo na kwamba wengi wao walitaka kupewa nafasi kuzungumza katika mazishi hayo.

Tabu ley aliyejulikana kama mfalme wa muziki wa rumba aliaga dunia mwezi uliopita mjini Brussels ,Ubelgiji akiwa na miaka sabini na sita.

Wengi walimkumbuka Tabu Ley kwa mziki wake na kwa talanta yake kwa utunzi wa nyimbo zake zilizowagusa watu wengi Afrika. Tabu Ley amefanyiwa mazishi ya kitaifa

Mwanamziki huyo ambaye pia alikuwa mwanasiasa, hakuwahi kupona tangu alipougua kiharusi mwaka 2008 na hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi alipofariki Novemba 30.

Alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji kimoja kidogo Magharibi mwa mkoa wa Bandundu, na hapo ndipo nyota yake ilianza kung'aa a katika fani ya muziki wa Rumba mapema miaka ya sitini.

Baadhi ya nyimbo alizoimba zilikuwa Adios Thethe na Mokolo nakokufa, na zilisaidia katika kufanya mziki wa Rumba kupendwa sana.

Tabu Lei alitaka sana kuwa waziri wa utamaduni katika serikali ya Laurent-Desire Kabila --babake rais Joseph Kabila, lakini badala yake akawa naibu gavana wa mji wa Kinshasa.

Alikimbilia usalama wake wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Mobutu Sese Seko kati ya mwaka 1965 to 1997, na mnamo mwaka 1990, serikali ya Mobutu ikapiga marufu album yake Trop, c'est trop.