Walinda amani 2 wa UN wauwa Mali

Image caption Waasi wa Azawad wamerejea vitani baada ya kutupilia mbali mkataba waliofikia na serikali miezi minne iliyopita

Walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulizi la bomu dhidi ya benki inayofanya kazi peke yake mjini Kidal Kaskazini mwa Mali.

Msemaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo, alisema kuwa shambulizi hilo lilifanyika mapema asubuhi kabla ya benki kufunguliwa.

Walinzi hao walikuwa wanalinda benki pekee inayomilikiwa na serikali mjini Kidal ambako waasi wa Tuareg wanataka kujitenga na Mali. Waasi hao walianza uasi wao miaka miwili iliyopita.

Shambulizi hilo linakuja kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wabunge.

Hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kundi la Azawad linalotaka kujitawala Kaskazini mwa Mali limesema kuwa linajiandaa kususia uchaguzi huo.

Mnamo mwezi Novemba, kundi la MNLA lilitupilia mbali mkataba wa Amani uliofikiwa kati yao na serikali miezi minne iliyopita na kuanza tena uasi.