1,200 wameuawa na Boko Haram tangu Mei

Image caption Boko Haram wamekuwa wakihangaisha watu katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria

Umoja wa mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 1,200 wameuwa katika mapigano yanayoendeshwa na wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini Mashariki mwa Nigeria tangu serikali kutangaza hali ya hatari mwezi Mei.

Kadhalika umoja huo umesema kuwa idadi hiyo inajumuisha raia na wanajeshi waliouawa na wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram katika majimbo ya Adamawa, Borno na Yobe.

Pia inajumuisha wapiganaji waliouawa na vikosi vya usalama.

Hii ni mara ya kwanza ripoti ya shirika la kujitegemea limetoa takwimu hizi tangu serikali kutangaza hali ya hatari.

Maelfu ta watu wameuawa tangu mwaka 2009, wakati Boko Haram walipoanza vita vyao dhidi ya serikali wakitaka kutawala Kaskazini mwa Nigeria kwa kutumi sheria za kiisilamu.

Kwa mujibu wa afisaa mmoja wa shirika la uratibu wa misaada la UN,takwimu hizo hazihusishi wapiganaji waliouawa katika harakati za jeshi dhidi ya kundi hilo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, hali nchini Nigeria hususan katika eneo la Kaskazini Mashariki, imekuwa ya kutia wasiwasi katika kipindi hiki cha mwaka 2013.

Kumekuwa na mashambulizi 48 yaliyofanywa na Boko Haram, katika eneo hilo tangu serikali kutangaza hali ya hatari.

Mnamo mwezi Mei, majimbo ya Borno,Adamawa na Yobe, yalitangaza sheria ya hali ya hatari. Nalo jeshi limekuwa likikabiliana na kundi hilo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Hata hivyo Boko Haram inaendelea na mashambulizi licha ya jeshi kupambana nao.