Aliyekuwa Meya Rwanda 'kudumu' gerezani

Image caption Kanisa la Nyange lilivamiwa na Watutsi 2000 waliokuwa wamejificha humo kuuawa

Meya wa zamani aliyepatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda ameongezewa muda wa kifungo chake kutoka miaka 15 hadi 25 katika kesi ya rufaa.

Gregoire Ndahimana alipatikana na hatia ya kukosa kuingilia kati wakati polisi chini ya ungalizi wake waliposhambulia kanisa moja ambako watu wa kabila la Tutsi walikuwa wametafuta hifadhi.

Ndahimana mwenyewe pamoja na upande wa mashitaka walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa kwanza.

Majaji wa rufaa waliongeza kifungho chake wakisema kuwa hakusaidia tu katika mauaji bali pia alisaidia katika kupanga mauaji hayo.

Takriban watu 800,000 wa Tutsi na wahutu wenye msimamo wa kadri, waliuawa katika mauaji hayo yaliyofanyika kwa siku miamoja mnamo mwaka 1994.

Wakati wa hukumu hio iliyotolewa katika mahakama maalum kuhusu kesi za Rwanda mjini Arusha Tanzania, meya huyo wa zamani aliketi chini nusura kuzimia huku mkewe akiangua kilio.

Zaidi ya watutsi 2,000 walikuwa wanatafuta hifadhi katika kanisa la kikatoliki la Nyange eneo la Kivumu wakati iliposhambuliwa na kuangushwa Aprili 16 , 1994.

Ndahimana pamoja na upande wa mashitaka walikata rufaa dhidi ya umauzi wa kwanza baada ya mahakama kumpata na hatia ya kuhusika na mauaji ya kimbare.

Inadaiwa alisherehekea na wenzake kwa kunywa pombe baada ya watu waliokuwa kanisani humo kuuawa.

Ndahimana alikamatwa nchini DRC mwaka 2009 wakati wa operesheni dhidi ya waasi kutoka Rwanda mashariki mwa nchi hiyo.