Wanawake na watoto wauawa DRC

Image caption Mashambulizi ya leo yameonyesha wazi changamoto inayokabili wanajeshi wa UN

Zaidi ya watu 20 wakiwemo watoto na wanawake wameuawa Mashariki mwa DRC , kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa.

Wengi walionekana kunyongwa Ijumaa na Jumamosi katika vijiji viwili katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ikiwemo wasichana watatu waliokuwa wamebakwa na kisha kukatwa vichwa.

Haijulikani nani aliyefanya mashambulizi hayo, lakini Umoja wa Mataifa unasema kuwa waliohusika lazima watachukuliwa hatua.

Takriban makundi 10 yaliyojihami yanaendesha uasi Mashariki mwa Congo.

Mashambulizi yalifanyika karibu na mji wa Beni, ambao uko umbali wa kilomita 250 Kaskazini mwa Goma.

Kwa mujibu wa kikosi cha umoja wa Mataifa kinachoshika doria DRC, (Monusco), mwathiriwa mwenye umri mdogo zaidi inasemekana alikuwa na miezi michache tu.

Wasichana watatu walionekana kubakwa na kukatwa kichwa. Mwili wa mtoto mdogo unasemekana ulikuwa umekatwakatwa kwa sehemu baadhi zikiwa zimewekwa mtini.

Baadhi ya maafisa wa kikosi hicho na wanaharakati katika mkoa wa Kivu Kaskazini, walituhumu kundi la (ADF-Nalu) la Uganda kwa kufanya mashambulizi hayo.

Kundi la ADF-Nalu linasemekana kuwa la kipekee lenya wapiiganaji wa kiisilamu katika eneo hilo.

Umoja wa mataifa una zaidi ya wanajeshi 19,000 nchini DRC huku sehemu ya kikosi hicho kikiwa kimepewa uwezo wa kuwashambulia waasi kwa silaha.

Wadadisi wanasema kuwa mauaji hayo yanaonyesha wazi changamoto zinazokabili kikosi cha Umoja wa Mataifa , licha ya kuwashinda waasi wa M23.

Serikali, ilitia saini mkataba wa amani na kundi hilo wiki jana. Waasi wa M23 walianza mapigano Aprili 2012 na kutuhumu maafisa wakuu kwa kuwanyanyasa wa Tutsi pamoja na kukosa kutii mikataba ya awali ya amani.