Milio ya risasi yatikisa Sudan Kusini

Image caption Rais Kiir amewalaumu wanajeshi watiifu kwa Riek Machar kwa kufanya jaribio la mapinduzi

Siku moja baada ya Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kusema kuwa serikali imefanikiwa kutibua jaribio la mapinduzi milio ya risasi imeendelea kusikika asubuhi ya leo.

Inaarifiwa milio hiyo ilikuwa inasikika kutoka katika moja ya kambi za jeshi mapema asubuhi ya leo.

Rais Salva Kiir alisema kuwa wanajeshi wake walitibua jaribio hilo la mapinduzi huku ripoti zikisema kuwa angalau mawaziri wanne wa zamani wametiwa nguvuni.

Miongoni mwa waliokamatwa ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani Gier Chuang, aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Oyai Deng Ajak , aliyekuwa waziri wa mazingira Alfred Lado Goro,na waziri wa zamani wa utamaduni Cirino Hiteng.

Mmoja wao Majak D'Agoot ameiambia BBC kwamba hawakutekeleza jaribio la mapinduzi ingawa walikuwa wamemkosoa bwana Kiir katika siku za hivi karibuni.

Hata hivyo haijulikani waliko makamu wa zamani wa rais Riek Machar na katibu mkuu wa chama cha SPLM aliyetimuliwa Pagan Ammum.

Wakati huohuo, Mjumbe maalum wa Marekani nchini humo, Donald Booth,ameambia BBC kuwa maelfu ya watu wametafuta hifadhi katika vituo viwili vya Umoja wa Mataifa mjini Juba.

Bwana Booth amesema kuwa uwanja wa ndege ulifungwa huku huduma za simu zikitatizwa.

Mnamo Jumatatu Rais Kiir, anayetoka jamii kubwa ya wa Dink, alilaumu wananajeshi watiifu kwa makamu wa rais wa zamani chini ya serikali ya Kiir Riek Machar kutoka katika kabila dogo la Nuer.

Wasiwasi wa kisiasa umeikumba Sudan Kusini tangu mwezi Julai baada ya bwana Kiir kulivunja baraza lake lote la mawaziri na kuwafuta kazi mawaziri wote akiwemo makamu wake wa Rais bwana Riak Machar.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii