Wanajeshi 6 wa US wafariki Afghanistan

Image caption Wanajeshi wa Marekani wanastahili kuondoka Afghanistan mwaka 2014

Wanajeshi sita wa Marekani wamefariki katika ajali ya ndege Kusini mwa Afghanistan.

Kwa mujibu wa kikosi cha kimataifa cha kutoa msaada wa kiusalama,(Isaf) , sababu ya ajali haijulikani na uchunguzi umeanza kufanywa.

Ripoti za awali zilisema kuwa hapakuwa na mashambulizi yoyote katika eneo hilo wakati wa ajali.

Maafisa kutoka katika wizara ya ulinzi nchini Marekani, walithibitisha uraia wa wanajeshi waliofariki.

Naibu gavana wa mkoa wa Zabul, aliambia shirika la habari la AP, kuwa halikopta za NATO, zilianguka katika eneo la Shajau.

Hata hivyo haijabainika ikiwa alikuwa anazungumzia ajali hiyo hiyo.

Mapema mwaka huu, Isaf ilikabidhi jukumu la kulinda usalama wa Afghanistan kwa wanajeshi wa nchi hiyo lakini wanajeshi wengine 97,000 hawajaondoka.

Kikosi cha NATO kina wanajeshi kutoka mataifa hamsini yaliyochangia wanajeshi wake ikiwemo wanajeshi wengine 68,000 kutoka nchini Marekani wanaotoa msaada wa kijeshi.

Ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014, wanajeshi wote wanapaswa kuwa wameondoka nchini humo.