Wabunge India wataka Marekani iwajibike

Image caption Waandamanaji India wakipinga ubalozi wa Marekani

Wabunge wa India wameelezea kusikitishwa na kitendo cha kumkamata na kumtendea vibaya mmoja wa wanadiplomasia wake mjini New York wiki iliyopita.

Kiongozi wa upinzani katika baraza la juu la bunge la India, Arun Jaitley amesema kukamatwa kwa balozi huyo ni ukiukaji wa mkataba wa Vienna.

Bi Devyani Khobragade, naibu balozi , alifungwa pingu na kupekuliwa akiwa amevuliwa nguo.

Bi Khobragade amekanusha tuhuma za udanganyifu wa viza na kutoa taarifa za uongo kuhusu tuhuma kwamba alikuwa anampunja mshahara mfanyakazi wake wa ndani.

Mfanyakazi huyo alilalamika kuwa balozi huyo alikuwa akimlipa kima cha chini cha mshahara kuliko kinachoelezwa katika viza ya Marekani.

Kufuatia kukamatwa kwake, Bi Khobragade alifikishwa mahakamani Ijumaa iliyopita na kuachiwa kwa dhamana.