Madaktari wauawa kwa shambulio Somalia

Image caption Moja ya majeruhi katika mlipuko uliotokea nchini Somalia

Madktari raia wa Syria na wa jamii ya kisomali wameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kufanyika shambulizi karibu na mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia BBC kuwa watu wenye silaha walishambulia gari lililokua likielekea katika hospitali moja.

Walinzi wao wawili pia waliuawa katika shambulio hilo, huku daktari mmoja wa Syria na mwingine wa Somalia walijeruhiwa .

Wanamgambo wa kiislamu, Al Shabaab wamekuwa wakisabisha hali ya usalama kuzorota nchini Somalia, hata hivyo haijathibitika ni nani anayehusika na shambulio hilo.

Madaktari wa Syria wanaelezwa kuwa walikua nchini Somalia kwa ajili ya shughuli za kutoa misaada.

Mwandishi wa BBC ameripoti kuwa shambulio hilo lilitokea katika wilaya ya Siinka Dheer inayodhibitiwa na Serikali, eneo lililo kusini mwa Mogadishu.

Madaktari waliojeruhiwa wako hospitalini wakipatiwa matibabu mjini Mogadishu, halikadhalika miili ya Watu sita waliouawa katika shambulio hilo wamefikishwa hospitalini.