Wapinzani Ukraine waja juu

Viongozi wa upinzani nchini Ukraine wamedai kufahamishwa ni jambo gani ambalo Rais Viktor Yanukovych, ameipatia Russia ili nchi yake ipatiwe msaada mkubwa wa kiuchumi.

Rais Vladmir Putin wa Russia amekubali kununua dhamana za serikali ya Ukraine zenye thamani ya mabilioni ya dola na pia kupunguza bei ambayo Ukraine inalipa kwa ajili ya nishati ya gesi kutoka Russia

Tangazo la makubaliano hayo limekuja wakati ambapo Russia inajaribu kuizuia Ukraine isijiunge na Umoja wa Ulaya, EU. Kiongozi wa upinzani, Vitali Klitschko, amewaambia waandamanaji wanaunga mkono EU kwamba, Bw. Yanukovych ameusaliti uhuru wa Ukraine.

"Ameacha kutetea maslahi ya taifa la Ukraine, ameusaliti uhuru," Bw. Klitschko, ambaye ni bingwa wa zamani wa ndondi ameuambia umati wa watu siku ya Jumanne. Ametoa wito kwa Rais wa Ukraine kuitisha haraka uchaguzi.

"yanukovych alisema katika meza ya mazungumzo kwamba haofii kufanyika mapema kwa uchaguzi. Kama ni hivyo, wacha athibitishe hilo kwa mpambano wa kiungwana," alisema.

Ingawa undani wa makubaliano hayo haujawekwa wazi, Bw. Oleh Tyahnybok, kiongozi wa upinzani wa kundi la mrengo wa kulia, amesema Bw. Yanukovych amegawa sekta zote za uchumi wa nchi kwa Russia.

Ukraine inahitaji kuziba haraka pengo la madeni yake ya nje yanayofikia kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 17 mwaka ujao, ili kuepusha kulimbikiza madeni yake.

Baada ya mazungumzo kati ya Bw. Putin na Bw. Yanukovych huko Kremlin, ilitangazwa kwamba, Russia itanunua dhamani za serikali ya Ukraine zenye thamani ya dola bilioni 15.

Marekani imeionya serikali ya Ukraine kwamba, makubaliano kati yake na Russia hayatawaridhisha waandamanaji..