Wageni waendelea kuondoka Sudan Kusini

Wageni  katika uwanja wa ndege wa Juba wakisubiri kuondoka

Mataifa ya nje yanaendelea kuwaondosha raia wao Sudan Kusini baada ya ghasia za kikabila za juma zima.

Makampuni ya mafuta ya Uchina yamekuwa yakiondosha wafanyakazi wake baada ya baadhi ya maeneo ya visima vya mafuta kuchukuliwa na watu waliokuwa na silaha.

Ndege ya pili ya jeshi la Uingereza iliondoka Juba ikibeba raia wa Uingereza.

Mamia ya watu wamekufa Sudan Kusini tangu ghasia kuripuka baina ya wanajeshi wa kabila la Dinka - wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir - na wale wa kabila la Nuer, watiifu kwa adui yake, Riek Machar.

Wakuu wanasema mawaziri kutoka nchi za jumuia ya IGAAD wanajaribu kuwasiliana na aliyekuwa makamo wa rais, Riek Machar, ili kujaribu kumaliza ghasia za kikabila zinazoendelea.

Hapo jana ujumbe huo ulikutana na Rais Salva Kiir, ambaye alikariri kuwa anataka kufanya mazungumzo na mpinzani wake Riak Machar.

Rais Kiir hakutoa shuruti yoyote.

Bwana Machar hajulikani aliko na amewahi kusema kuwa yuko tayari tu kujadili kujiuzulu kwa rais.

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, anamtuma mjumbe wake maalum, Donald Booth, kwenda Juba kujaribu kuhimiza mazungumzo.

Mashambulio kwenye mitambo ya mafuta katika jimbo la Unity, kando ya mpaka wa Sudan, yameleta wasi-wasi kuwa uchimbaji wa mafuta unaweza kusimama kabisa katika nchi ambayo pato lake kubwa linatokana na mafuta.

Vyombo vya habari vinasema wafanyakazi zaidi ya 16 kwenye sekta ya mafuta wameuwawa na mamia wamekimbia.