Majeshi ya AU yaua mtu mmoja CAR

Image caption Askari wa Ufaransa akiwatuliza waombolezaji,CAR

Majeshi ya Umoja wa Afrika, AU, yamewafyatulia risasi waandamanaji katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR, na kumuua mtu mmoja.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema watu 40 pia walijeruhiwa katika tukio hilo, wengi ikiwa ni kutokana na kukanyagana, kulikosababishwa na kufyatuliwa kwa risasi karibu na uwanja wa ndege mjini Bangui.

Jumapili askari wa Ufaransa waliwaua watu watatu, imesema serikali ya CAR.

Majeshi ya AU na Ufaransa yanapambana kukomesha mgogoro kati ya Wakristo na Waislamu ambao umeikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wapiganaji kutoka pande mbili hizo wamehusika katika mashambulio na kulipiza kisasi tangu Bwana Michel Djotodia ajitangaze kuwa Muislamu wa kwanza mtawala wa nchi hiyo mwezi Marchi, akimtoa madarakani aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize, ambaye anatoka katika kundi la Wakristo walio wengi nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la Amnesty International, siku mbili za ghasia mapema mwezi huu zilisababisha watu wapatao 1,000 kuuawa.