Dunia yaupokea mwaka mpya 2014

Image caption Sehemu ya sherehe za mwaka mpya 2014,Sydney,Australia

Maelfu ya watu duniani wanajiandaa na sherehe za kuupokea mwaka mpya wa 2014, huku katika mji wa Sydney nchini Australia wakiwa tayari wamekwisha upokea mwaka mpya wa 2014 kuliko maeneo mengine yote duniani na sherehe za kijadi zinaendelea kwa ajili ya sherehe hizo.

Nchini Japan ambao nao tayari wamekwishaupokea mwaka huu saa mbili nyuma ya Australia, hivi sasa viongozi dini ya kijadi ya Shinto wamekusanyika katika mahekalu ya dini hiyo kwa ajili ya sherehe za mwaka mpya. Miji mingine pia duniani inatarajia kuupokea mwaka mpya kwa sherehe kubwa ambapo katika mji wa Dubai, Falme za Kiarabu wanatarajia kuvunja rekodi kwani sherehe hizo zitaonyeshwa moja kwa moja katika mitandao ambapo pia miale ya milipuko ya fataki inatarajiwa kwenda hewani umbali wa kilomita 48.

Nchini China sherehe zikitarajiwa kufanyika katika miji yake iliyo mingi, lakini katika mji wa Wuhan wamesitisha harakati za sherehe hizo ili kuepusha uchafuzi wa mji. Hata hivyo katika miji mingine ya nchi za Ulaya sherehe kubwa zitafanyika pia katika miji mbalimbali ikiwemo, Moscow, Paris na London.

Nchini Afrika Kusini maandalizi yamefanyika ili kuwa na tamasha la wazi maalumu kwa ajili ya kumuenzi kiongozi wa taifa hilo, Hayati Nelson Mandela aliyefariki dunia Desemba 5 mwaka 2013.

Katika mji wa New York wao wataukaribisha mwaka mpya kwa utamaduni wao wa milio ya saa kwa kuhesabu muda uliobaki pamoja na midundo ya mpira. Na katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil kwa mara nyingine watu zaidi ya milioni mbili watakusanyika katika ufukwe wa Bahari wa Copa Cabana.

Katika nchi za Afrika Mashariki, maandalizi yanaendelea kwa waumini wa dini mbalimbali kwenda katika nyumba za ibada, kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kumaliza mwaka 2013 na kuupokea mwaka mpya wa 2014.

Uongozi wa BBC unawatakia watazamaji, wasikilizaji na wasomaji wake Heri ya Mwaka Mpya wa 2014.