10 wajeruhiwa katika shambulio Kenya

Ramani ya Kenya ikionyesha mji wa Mombasa
Maelezo ya picha,

Ramani ya Kenya ikionyesha mji wa Mombasa

Watu wapatao 10 wamejeruhiwa katika shambulio la gruneti katika kituo kimoja cha utalii, kusini mwa mji wa Mombasa nchini Kenya.

Kwa mujibu wa polisi washambuliaji hao walirusha gruneti hilo katika baa ya Tandoori katika mji wa Diani, mapema asubuhi, Alhamisi.

Polisi wamesema waliojeruhiwa walipelekwa hospitali na hali za afya zao ni thabiti.

Pwani ya Kenya, yenye mchanga na fukwe nzuri, ni maeneo yanayowavutia watalii, lakini yamekumbwa na matukio ya mashambulio yanayohusishwa na wapiganaji wa Kiislam.

Hakuna mtu wala kundi lililodai kuhusika na shambulio la Alhamisi.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo Jack Ekakuro amewaambia waandishi wa habari kwamba baa ya Tandoori ilijaa watu waliokuwa wakisherehekea Mwaka Mpya wakati shambulio hilo lilipotokea majira ya saa 9:30 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki.

"Watu watatu walionekana wakitokea upande wa pili wa barabara na kutupa gruneti katika klabu hiyo ya usiku, ambapo lililipuka na kujeruhi watu 10, amesema kamanda wa polisi." "Washambuliaji hao walikimbia kwa kutumia pikipiki".

"Hakiwezi kuwa kitu kingine chochote kile lakini ni shambulio la kigaidi," aliendelea kusema.

Maeneo ya kitalii mjini Mombasa yamekuwa yakilengwa na mashambulio ya kigaidi.

Watalii wawili kutoka Uingereza waliokuwa wakisafiri kati ya Diani na Mombasa walinusurika kufa mwezi Desemba, baada ya gruneti walilorushiwa katika gari lao kushindwa kulipuka.