Pervez Musharraf alazwa hospitali

Image caption Pervez Musharraf, rais wa zamani wa Pakistan

Mtawala wa zamani wa kijeshi nchini Pakistan, Pervez Musharraf amelazwa hospitali kwa kile kinachoshukiwa kuwa ni matatizo ya moyo, akiwa njiani kuelekea mahakamani ambako anakabiliwa na mashitaka ya uhaini.

Maafisa nchini Pakistan, wameiambia mahakama kuwa Musharraf mwenye umri wa miaka 70, alihamishiwa katika hospitali ya kijeshi ya magonjwa ya moyo huko Rawalpindi.

Hii ni mara ya tatu kwa rais huyo wa zamani wa Pakistan kushindwa kufika mahakamani kufuatia matukio mawili yaliyopita kuhusishwa na wasiwasi kutokana na hali ya usalama.

Mashitaka ya uhaini yanahusishwa na uamuzi wake wa mwaka 2007, kusitisha katiba na kutangaza hali ya hatari.

Bwana Musharraf amekana mashitaka hayo na anasema tuhuma zote dhidi yake zinatokana na msukumo wa kisiasa.