Vita vyachacha mazungumzo yakipangwa

Image caption Watu waliokimbia makaazi yao kutokana na vita nchini Sudan Kusini, wakisubiri maboti kuvuka mto Nile, katika mji wa Bor.

Mapigano yanaendelea nchini Sudan Kusini licha ya pande mbili zinazohusishwa na mgogoro wa nchi hiyo kujiandaa kwa mazungumzo ya amani nchini Ethiopia.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini ameiambia BBC kuwa mapigano yanaendelea katika mji wa Bor na baadhi ya sehemu za jimbo la Unity.

Pande zote mbili za serikali na waasi wamepeleka wajumbe wao katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Mpaka sasa waasi wamekataa kusitisha mapigano, wakati mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo yakiendelea.

Mashirika ya misaada yamesema msaada wa dharura unahitajika haraka kwa maelfu ya watu waliolazimika kuyakimbia makaazi yao.

Hali imezidi kuwa mbaya katika kambi ya wakimbizi ya Awerial iliyopo katika kingo za mto Nile- ambako sasa ni makaazi ya watu 75,000 waliokimbia mapigano jirani na Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei, ambalo kwa sasa linadhibitiwa na waasi. Mji wa Bor umekuwa ukibadilishwa udhibiti wake kati ya majeshi ya serikali na waasi, kutokana na umuhimu wake. Mara ya kwanza ulitwaliwa na waasi, lakini ukakombolewa na majeshi ya serikali na sasa umerudi tena mikononi mwa waasi.

"Hakuna maji safi ya kunywa. Visima vitano- havitoshi," David Nash wa shirika la madaktari wa MSF ameiambia BBC.

"watu wanakunywa maji moja kwa moja kutoka mto Nile. Yna matope, si mazuri. Na hakuna vyoo, kwa hiyo magonjwa ya kuambukiza yanajitokeza. Kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, ni hali inayowezekana kabisa kutokea.