Unene kupindukia katika nchi zinazostawi

Image caption Unene kupinduikia ni tatizo linalokita mizizi katika mataifa yanayostawi

Kunenepa kupindukia ni tatizo ambalo sasa linatishia zaidi maisha ya wengi katika mataifa yanayostawi duniani kuliko katika mataifa tajiri ambako mambo yana afadhali.

Sasa serikali nyingi zinaombwa kuongeza Ushuru vyakula hivyo vinavyosababisha watu kunenepa kupindukia kama njia ya kuokoa maisha ya watu kutokana na mshutoko wa moyo, kisukari na kiarusi.

Kutokana na takwimu za kimataifa, kila mtu mmoja kati ya watatu wazima duniani, anatambuliwa kama aliyenenepa kupita kiasi. Mwaka 1980 takwimu hiyo ilikuwa kila mtu mmoja kati ya watano.

Ripoti ya Shirika la utafiti wa matumizi ya chakula la The Future Diets, lilikagua takwimu zilizopo na kugundua kuwa ongezeko la watu wanene kupindukia limetokea katika mataifa yanayostawi kama vile Mexico na Misiri, ambako watu wanatumia utajiri wao wa ziada kula vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi.

Katika muda huo idadi ya wanene ilipanda mara tatu kutoka Milioni 250 hadi Milioni 904.

Ripoti hiyo inasema kwamba mataifa yaliyostawi ambayo yamekuwa na changa moto nyingi zaidi kuhusiana na maswala ya unene yameshindwa kuthibiti kikamilifu maswala yanayohusiana na hali hiyo.

Ripoti hiyo imemulika kampeni iliyofaulu nchini Korea Kusini ambako wanawake wanafunzwa jinsi ya kutengeneza vyakula kiasili ambapo mafuta madogo zaidi yanatumika.

Wanawake wawili waliopatikana katika kibanda cha kuuza matunda katika mji mkuu wa Korea Kusini wa Seoul waliambia BBC sababu za wembamba wao. Mmoja alisema hana wasiwasi wa kunenepa kwa sababu yeye hupenda kunywa uji, mboga na matunda.

Mwanamke wa pili alisema kuwa raia wengi wa Korea wanapenda mboga zaidi, ambapo wenzao kutoka mataifa ya Mahgaribi hupendelea kula nyama ya Ng'ombe. Mama huyo alisema pia kuwa kwa kawaida raia wa Korea kwa ujumla hula chakula kidogo zaidi kwa sababu wanajali zaidi unene wao.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa mataifa mengi yanapaswa kutoza kodi kubwa vitamutamu kama vile soda na peremende.

Ripoti hiyo ya The Future Diets inasema kuwa iwapo mienendo ya ulaji wa sasa itaendelea kutakuwepo na ongezeko zaidi la mshtuko wa moyo, kiharusi na ugonjwa wa sukari.